Praise The LORD!
Mungu yu mwema kila wakati....
Leo tuongee kidogo kuhusu mafanikio.Kuna mafanikio yanayotoka kwa Mungu na yale yatokayo kwa yule mwovu,ibilisi.Mafanikio yanayotoka kwa Mungu huwa yanadumu,maana yana ulinzi wa Mungu ndani yake,hayana masharti.Nira ya Mungu ni laini Mathayo 11:29-30 tunaona Bwana Yesu anawaasa ya kuwa wajifunze kutoka kwake,maana yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo na kwamba watapata raha nafsini mwao,maana nira yake ni laini,na mzigo wake ni mwepesi. Mungu ni BaBa mwenye upendo.Akikubariki anafanya hivyo kwa moyo wake wote.Anakubariki baraka za rohoni mpaka za mwilini pia,anakupa amani wakati wote.
Lakini haya yote hayaji hivi hivi tu,kuna gharama za kulipa lakini gharama hizi ni nyepesi sana.Sio kama za shetani,ambazo ni ngumu sana,nzito,zinazogharimu maisha ya wapendwa wako kila mara,halafu mafanikio yenyewe hayadumu,tena yana masharti yasiyofaa, ya kudhalilisha.
Katika kitabu cha Yoshua 1:7-9 BWANA alikuwa anaongea na Yoshua baada ya Musa kufa akamwambia,
7 Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako.
8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.
9 Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.
Mambo makuu matatu(3) Tunayotakiwa Kufanya
1) Tunakiwa kuwa hodari na wenye ushujaa mwingi.
Ina maana kuelekea kwenye mafanikio utakutana na vikwazo vingine vinakaribia kukatisha tamaa kabisa maana kumbuka kwanza shetani hapendi uwe levo nyinigine ya juu.
Mungu alimsisitiza Yoshua ya kwamba awe hodari na mwenye ushujaa mwingi.Kwa kifupi Mungu hapendi mtu uwe na tabia ya woga maana kwanza woga hautokani naye.2 Timotheo 1:7 inasema
'Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi'.
2)Uangalie na kutenda sawasawa na maandiko yanavyosema,usigeuke kulia wala kushoto.Kwa maana nyingine usipindishe chochote.Hapa sasa ndio tuulizane.Tunasoma maandiko kila siku?Tunayaelewa vizuri?Tunayatafakari mchana na usiku kuyazamisha kwa kina kwenye mioyo yetu?
Hivi unafahamu maandiko ndiyo mwongozo wote?Kuna majibu ya mambo yote chini ya jua kupitia maandiko ambalo ni Neno la Mungu lililo hai.Ndio maana mtunga Zaburi aliona hili na akasema wazi katika Zaburi 119:105 ya kwamba
105 Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
Usiposoma maandiko unajuaje haki zako?Unajuaje namna ya kumshinda shetani?Unajuaje mambo unayotakiwa kufanya na usiyotakiwa kufanya?Mungu anazungumzaje nawe?japo zipo njia nyingi ambazo huwa anatumia lakini hii huitumia sana maana ni lazima athibitishe kila asemalo kupitia Neno lake au maandiko.Kwa kifupi kama hatusomi Biblia,tuanze.Kuna majibu ya maswali yote chini ya jua.Roho Mtakatifu ni mwalimu mzuri sana.Atakufundisha,utaelewa.Maana Biblia si kitabu mtu akisoma anakielewa kirahisi.Lakini ukishampokea Bwana Yesu na Roho Wa Mungu akawa ndani yako,anakufundisha unaelewa vizuri sana.
3)Uwepo wa Mungu kwenye maisha yako.Tunaona kwenye mstari wa 9 hapo juu Mungu alimhakikishia Yoshua kwamba yupo pamoja nae kila aendako.Na Mungu akiwa upande wako ni nani anaweza kuwa kinyume chako?
Sasa swali kwetu,umeshamkiri Bwana Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako?Maana ukishamkubali tu,anatembea pamoja nawe kila uendako na ndio mwanzo wa kufanikiwa maana YeYe,Mungu Baba na Roho Mtakatifu watafanya makazi ndani yako na watakuongoza na kila unapotii na kufanya vile Roho Mtakatifu anavyokuamuru,utafanikiwa.
Barikiwa sana.
Mpaka wakati ujao,
TANZANIA KWA YESU!