Wakristo wote ulimwenguni tunatambua ya kwamba tunaelekea pasaka,siku ambayo tunaadhimisha kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Leo ni ijumaa kuu,siku ambayo imetengwa ulimwenguni kwa ajili ya kukumbuka mateso aliyoyapata Bwana wetu Yesu Kristo pale msalabani ili atuokoe sisi kutoka katika vifungo vya dhambi na laana.
'Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,Alichubuliwa kwa maovu yetu;Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake,Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona'(Isaya 53:5).Vile vile (1Petro 2:24) inazungumzia jambo hilo hilo ya kwamba 'Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti,tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi,tuwe hai kwa mambo ya haki;na kwa kupigwa kwake mliponywa.
Leo ni tunakumbuka siku ambayo tulikombolewa rasmi.Kwa kifupi,tumewekwa huru na dhambi.Hatuko tena chini ya sheria wala dhambi haipaswi kututawala.Tunapata nguvu ya kuishinda dhambi pale tunapomkaribisha Bwana Yesu mioyoni mwetu.
Ni muhimu sana tukajitafakari Yesu ana nafasi gani maishani mwetu.Ikiwa tunamaanisha kumpenda Bwana Yesu basi tubadilike.Hatutakiwi kulia leo,wala kuomboleza,wala kuvaa nguo nyeusi zaidi ni tubadilike mioyoni kwa kumkubali na kukiri ya kwamba alitufia msalabani na siku ya tatu akafufuka katika wafu (Warumi 10:9-10).Mungu haangalii mwili kama ambavyo sisi tunaangalia.Mungu anaangalia roho yako. Je,roho yako inamwamini,kumkiri na kumcha kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.Angalia hata katika suala la kuabudu,Mungu anatafuta wale wamwabuduo katika roho na kweli maana Mungu ni Roho. (Yohana 4:24). Kwa kufanya hivyo utaokoa nafsi na roho yako kutoka kwenye jehanamu ya milele.
Ushindi, uponyaji, uzima wa milele na mengineyo unapatikana tu baada ya kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu.Kinyume na hapo shetani atakuonea sana.Atakutesa na magonjwa, mikosi, mabalaa, hutafurahia maisha utatamani kuondoka kabla ya muda wako lakini fahamu ya kwamba Yesu alikuja ili tuwe na uzima kisha tuwe nao tele.(Yohana 10:10)
Haya mambo ya kusema ni mipango ya Mungu mtu unapopata mabalaa,shida,magonjwa na maonevu kwa kweli hebu tuamke.Hivi ni yupi kati yetu ambaye ana sifa kamili za kuitwa mzazi akawa anamtesa na kumtenda vibaya mwanaye wa kumzaa?Na ukiona mwanadamu anayefanya hivyo ujue hana sifa kamili za kuitwa mzazi.Ndiyo maana hata maandiko yalisema mama anaweza kusahau kunyonyesha mwanae mchanga lakini Mungu hatakusahau wewe.Pia lingine linatoka katika Mathayo 7:11 linasema 'Basi,Ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema,Je,si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni?atawapa mema wale wamwombao?
Lakini mzazi mwenye akili timamu na anayejitambua huwapenda wanawe na kuwasaidia.Mtoto mwenye mahusiano mazuri na mzazi wake huwa anafaidi sana.Tuangalie hata uhalisia.Mnaweza mkawa mmezaliwa watatu kwa mfano,au wewe ukawa na watoto watatu au hata wawili lakini yule ambaye ni mtiifu na ana mahusiano mazuri na wewe ndiye kipaumbele chako.Akiita tu,ushafika kabla hata hujaitika.Na Mungu ndiyo hivyo.
Tengeneza mahusiano yako na Mungu sawa kwanza,ili uweze kurithi haki zako,uwe na mamlaka na Ibilisi na pia akuitikie pale unapomwita.
Kwa leo naishia hapa..Tukutane tena wakati ujao.
TANZANIA KWA YESU!
No comments:
Post a Comment