Thursday, April 24, 2014

Usikate Tamaa Wewe Ni Askari Vitani



Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.(Yohana 16:33b)
Hayo ni maneno ambayo Bwana Yesu aliyazungumza mwenyewe.Hii dunia tunayoishi,sio kila wakati itakuwa ni haleluya,tambarare.Kuna wakati milima mikubwa inajitokeza katika maisha yetu.

Hata Bwana Yesu mwenyewe alijaribiwa na shetani.Tunaona hayo katika Neno La Mungu (Mathayo 4:1-11)
Mambo machache tunayogundua hapa ni:

1.Roho wa Bwana alimpandisha Yesu nyikani ili ajaribiwe na Ibilisi

2.Yesu alipoanza kuona njaa baada ya kufunga siku arobaini mchana na usiku,shetani akaona ni fursa ya kumjaribu

3.Yesu alimshinda Ibilisi kwa kutumia maandiko.

4.Shetani aliendelea kumjaribu mara nyingine kadhaa

5.Yesu alishinda majaribu YOTE.

6.Unaposhinda Mungu hutuma malaika zake kukuhudumia.

          
Si kila mara unapoingia kwenye jaribu ni Roho wa Bwana kakuongoza.Kuna wakati tamaa zetu wenyewe zinatuongoza.Tuangalie Yakobo 1:13-14 ' 13Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu.
14 Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa'

Pia tunagundua shetani anatusoma mno akitafuta fursa ya kutujaribu.Anaangalia pale utakapokuwa na ka-udhaifu labda unatamani kitu fulani ndiyo anatengeneza mazingira ya kutujaribu.Mfano,labda ulikuwa una tabia ya kusogeza vitu vya wengine kimya kimya(kibaka).Pale ambapo utakiri na kujiamulia kutoka kwenye kina cha moyo kwamba hutaiba tena,utashangaa mazingira yatakayokuzunguka.Vitu vya watu vitaachwa vinaranda hovyo na hapatakuwa na mtu ila wewe na Mungu wako.

Kingine ni mara nyingi unapoamua kumtafuta Mungu kwa kumaanisha,ukafunga ukaomba kuutafuta uso wa Bwana kwa muda mrefu,kama umefuatilia kwa karibu ukitoka hapo tu mara nyingi unakuta shetani ameshatayarisha kitu cha kukujaribu.Inabidi tuwe makini sana pindi tunapotoka kuutafuta uso wa Bwana maana ibilisi anajua vizuri madhaifu yako na yangu.Atatumia chochote kukujaribu.Kama ni mtu wa hasira za haraka basi atatafuta chanzo chochote cha kukulipua hasira.Inapaswa kumshinda.
 Ndiyo maana Bwana Yesu alipokuwa anawafundisha wanafunzi wake kusali aliongezea ' ..Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu.' (Mathayo 6:13)
Alijua fika yule mwovu hachezi mbali na sisi.Kama hakuona aibu kumjaribu Bwana Yesu hataona aibu kutujaribu mimi na wewe.Ni vizuri pia kuomba sala hii ya ulinzi wa Bwana juu ya majaribu kila mara unapoomba,maana Bwana Yesu alifahamu hila za mwovu juu yetu.

Bwana Yesu alitumia Neno la Mungu kumshinda ibilisi.Huyu ibilisi anayajua vizuri tu maandiko,anachofanya yeye ni kuyatumia kwako ndivyo sivyo au akipindisha mwingine.Unatakiwa kujua vizuri sana maandiko na namna ya kujisimamia.Ndiyo maana tumeambiwa Neno la Mungu lijae kwa wingi mioyoni mwetu, pia tuweke Neno la Mungu sana mioyoni mwetu tusije tukamtenda dhambi(Zaburi 119:11)



Shetani huwa hakati tamaa.Lazima atakuzungukia mara kadhaa kama alivyomzungukia Yesu.Atakaa pembeni kwa muda kidogo kisha atarudi.Yatupasa kuwa macho na kuyashinda majaribu Yote.

Baada ya hapo ukishinda,Mungu hutuma malaika zake kukuhudumia.Yale yote uliyoyaomba unayapata,wakati mwingine na ziada pia.Mungu ni Pendo.

Kwa hiyo ndugu yangu,shetani akikuletea,mpe za kutosha.Mtusue kweli kweli.Mpe majeraha ya nguvu,akae kwenye 'koma' karne zote zilizobakia.Ifike mahali ajishauri kuja kuleta pua yake kwako.Mambo ya shetani sijui alijiinua sijui nini hakuna kitu kama hicho.Labda kama unataka kumwinua.Lakini una uwezo wa kumdunda kisawasawa mpaka akawa anajishauri kukuingia.Na Mungu hupenda watu jasiri.Hivi unafahamu wa kwanza kutupwa kwenye ziwa la moto ni WAOGA?soma Ufunuo 21:8



Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.(Yakobo 1:12)

Pamoja na yote, kitabu cha 1Wakorintho 10:13 ' Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.'

Jipe moyo mkuu ndugu yangu unapopitia majaribu.Usikate tamaa.Cha kwanza ni uchunguze moyo wako endapo kuna dhambi yoyote unayoifahamu umetenda,itubu.Tubu hata zile usizozifahamu.1Yohana 1:8-10  inasema ' 8Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.'

Usilie


Mungu ni mwema na mwaminifu mno .Anasamehe.Cha kwanza kabisa hakikisha umempa Bwana maisha yako,then mpende sana,kaza sana kumpenda na kuzishika amri zake,soma sana Neno lake ili uijue kweli na uweze kumshinda yule mwovu,halafu uwe muombaji mzuri uone Mungu atakavyokuokoa,atakavyokuwa nawe taabuni,atakavyokutukuza na kukushibisha siku nyingi.n.k..

Zaburi 91:14-16 imeeleza hapa chini:
14 Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu.
15 Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;
16 Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu.


Somo ni refu,ila kwa leo naishia hapa..

TANZANIA KWA YESU! 

Nakuachia wimbo huu,Usikate Tamaa by Martha Mwaipaja




No comments:

Post a Comment