Thursday, June 5, 2014

Kwa Nini Kuogopa Wakati Unaweza Kuomba?



Luka 18:1
1 Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.

Bwana Yesu akaendelea kutoa mfano kwenye Luka 18:2-14
Haya maneno yalitoka katika kinywa cha Bwana Yesu mwenyewe.Ni maneno ya Mungu mwenyewe.Mungu anaelewa tunapaswa kuomba,kwa sababu Bwana Yesu naye aliishi duniani kama sisi,anaelewa mahitaji yetu na changamoto tunazokutana nazo,naye mwenyewe alikuwa ni mwombaji.

Maombi ndiyo njia pekee ambayo Mungu ameichagua sisi kuwasiliana naye kumwambia mahitaji yetu na mambo yetu yote.Ni njia aliyoichagua ya sisi kuwasiliana na YeYe.Hakuna njia nyingine yoyote ambayo mwanadamu anaweza kuwasiliana na Muumba isipokuwa kupitia maombi.

Ukienda kuwasiliana na Mungu,jisafishe,jitakase,nyenyekea,ongea naye kirafiki na kwa heshima kama unaongea na baba yako.Mungu hapendi woga,kulalamika,kunung'unika yani anachukia kabisa.Unakumbuka wana wa Israel walipokuwa njiani kuelekea Kaanani wale waliokuwa wananung'unika na kulalamika Mungu aliwafanyaje?Soma Kutoka 16. 




Haya yote yameandikwa ili iwe onyo kwetu.Kwa wale ambao tuna wepesi wa kulalamika,kunung'unika,kumtupia Mungu lawama,ukipatwa na mabaya au ukiwa kwenye hali ngumu sana unasema ni mpango wa Mungu jamani TUACHE.Kuna wakati mambo magumu yanakupata kupima imani zetu,wakati mwingine ni sababu ya dhambi zetu wenyewe n.k.

1Wakorintho 10:10-11
'10 Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.
11 Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. '

Wengi wetu tunapokuwa kwenye kipindi kigumu katika maisha,huwa tunalalama,kunung'unika,kusikitika yani hayo yote hata ufanye kiasi gani Mungu hakuangalii wala hakusikilizi,ndio tujue ni kiasi gani Mungu anachukia haya.Ni pale tu,unapomuendea na kumwomba,ndipo anapokusikiliza.

Mathayo 7:7-11 inasema,
'7 Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;
8 kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
9 Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe?
10 Au akiomba samaki, atampa nyoka?
11 Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?'



Hivi hata kama ni wewe,una watoto wako wawili.Mmoja yeye akiwa na uhitaji anakufuata,anakueleza halafu anakupa muda ulitendee kazi hitaji lake.Mwingine,yeye akiwa na hitaji hakwambii,utasikia tu kwa watu au utamsikia huko nje analalamika,ananung'unika hivi huyu ungependa kumsaidia kweli?Kama hajakufuata kukuomba yeye binafsi utamsaidia kivipi?Ndivyo ilivyo kwa Baba Yetu wa Mbinguni.Ana hisia jamani,inabidi tuwe makini tumtendee haki.

Somo hili litaendelea...Mpaka wakati ujao..
TANZANIA KWA YESU!




No comments:

Post a Comment