Thursday, May 29, 2014

Amri Kuu Ya Kwanza Ni Ipi




Marko 12:28-30
28 Na mmojawapo wa waandishi akafika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?
29 Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja;
30 nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.

Hapa tunaona ya kwamba:
1.Bwana Mungu wetu ni Mmoja.
2.Tunapaswa kumpenda kwa Moyo Wote,Roho Yote,Akili Yote,Nguvu Zote.

Tujiulize kiuhalisia,ukiwa unampenda mtu fulani kweli kutoka moyoni unakuwa katika hali gani.Yawezekana
1.Unawasiliana naye mno kuliko watu wengine ulionao kwenye maisha yako
2.Unamtafakari mara kwa mara sana
3.Unapenda kumfurahisha,unamheshimu na hupendi audhike
4.Unatenga muda kukaa naye kuongea,kucheka,kufanya chochote pamoja naye
5.Unatumia nguvu zako nyingi kushirikiana naye n.k..n.k..



Ndivyo hivyo tunavyotakiwa kumtendea Muumba wetu na kuzidi maana kwanza YeYe Ni MUNGU,Anastahili.Hiyo peke yake ni sababu tosha ya kumpenda.

1.Tunatakiwa kuwasiliana naye mno kuliko mtu mwingine yoyote kwa kusoma Neno lake na Kuomba.Kusoma Neno lake ni mojawapo ya njia ya kusikia sauti yake juu mambo yako binafsi,familia au jamii inayokuzunguka.Mungu hutumia sana Neno kuzungumza na watu wake.Ndiyo maana tumeambiwa Neno la Mungu likae kwa wingi mioyoni mwetu...(Wakolosai 3:16) Kuna nguvu kubwa sana katika kusoma Neno la Mungu na shetani kwa kulijua hilo ANAPINGA SANA  sisi kusoma Neno.




Kufanikiwa kwetu na kutofanikiwa kimwili na kiroho kunategemea sana kufuata sheria za Mungu kupitia Neno lake ( Yoshua 1:8)
'8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. '

2.Unamtafakari Mungu?Ukuu wake,uweza wake,uwepo wake,n.k .Tukimfahamu Mungu vizuri,hata changamoto tunazokumbana nazo kwenye maisha utaona ni sisimizi,nothing mbele za Mungu na amani yetu inakuwa tele.Hebu tujitengee tabia ya kumtafakari Baba Wa Mbinguni na sheria zake.(Zaburi 1:2 )
 '2 Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.'

3.Tunamheshimu Mungu na hatupendi audhike.Je,tunashika amri zake?maana Bwana Yesu alishasema 'Mtu akinipenda,atazishika amri zangu (Yohana 14:15) ikaendelea mbele kusema naye Mungu atakuja kamili kufanya makao ndani yako.Mungu akiwa ndani yako huwi mtu wa kawaida katika ulimwengu wa roho na mwili.Kwa macho unaonekana binadamu wa kawaida lakini ndani yako una nguvu na mamlaka ya ajabu mno.

Somo hili litaendelea...Mpaka wakati ujao,

TANZANIA KWA YESU!

Sunday, May 25, 2014

Kumshukuru Mungu



Zaburi 95 , 96 , 100

Praise The Lord!

Leo nimeamka nikatulizana hapohapo kitandani kimya nikamtafakari Mungu.Nikaanza ku-analyse jinsi anavyoshughulika na maisha yangu,familia yangu,jinsi anavyoshughulika na kazi zangu,biashara zangu,watu walio karibu yangu,kwa kweli moyo wangu uliishia kumshukuru kwa machozi ya furaha.




Mungu ni mwema sana.Anajishughulisha mno na maisha yetu.Amejaa upendo juu yetu na anahurumia sana wanaomcha YeYe.(Zaburi)

Tuna kila sababu ya kumshukuru sana Mungu.Uzima/Uhai,nguvu,Furaha,Amani,afya njema na mengineyo ni sababu tosha ya kumshukuru Mungu.Mimi nimemuona binafsi akishughulika na maisha yangu kila siku.Kila jambo ninalotaka kufanya huwa namshirikisha,nikipata amani kutoka kwenye kina cha moyo nalifanya.'Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo ninyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani!(Wakolosai 3:15)

Shukrani ni sehemu ya maombi.'Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; '(1Timotheo 2:1). Ni vyema ukatanguliza shukrani zako mbele za Baba,mwambie jinsi unatambua uwepo wake na msaada wake katika maisha yako,mwambie jinsi alivyo mkuu n.k.Yeye ni Mungu,Muumba wa Mbingu na nchi,na vyote, na itabaki kuwa hivyo, hiyo tu ni sababu tosha ya kumshukuru achilia mbali mengine aliyotubariki.Anastahili.




Kumshukuru Mungu ni muhimu nyakati zote maana kuna nyakati chini ya jua Mhubiri 3:1-8. Unapokuwa mtu wa shukrani,moyo wa Mungu unafurahi.Hata kama ni wewe una mwanao mmoja huyo yeye ukimpa pipi anakushukuru kama vile umempa gari,na ukimpa gari anakushukuru vizuri sana kwa kiwango hicho hicho nadhani ungempenda sana tofauti na yule ambaye ukimpa pipi hashukuru.Huyo ana dalili hata ukimpa gari ataona ni kawaida tu.Hatashukuru.'Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. '(Mathayo 25:29)



Hata ndege asubuhi huamka na nyimbo za furaha na shukrani.Kumbuka sana kumshukuru Mungu kila unapoamka na kabla ya kulala.Hata kwa maneno machache tu,kama umechoka sana.Baba yetu ni muelewa mno.

Nitaendelea...Nakuacha na wimbo 'When I think of You' by Michael W Smith.




Oh! napenda hiyo chorus yake..Yahweh!There is no one like You Lord
                                                     Yahweh! Halelujah, we sing,
                                                     Yahweh!There is no one like You Lord 
                                                     Yahweh!Your banner for me,Your banner for me,is LOVE!

Mpaka wakati ujao,

TANZANIA KWA YESU!



Wednesday, May 21, 2014

Jizungushie Watu Chanya Katika Maisha Yako



Mithali 13:20
20 Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

Yes.Unapaswa kuwa makini mno mno na mtu/watu unaowakaribisha kwenye maisha yako.Mafanikio yako ya kimwili na kiroho yanaathiriwa na mtu au kundi linalokuzunguka.Hupaswi kuwachukia wasio na hekima au 'wapumbavu',kama biblia inavyowaita,bali usiwafanye rafiki zako.

Kuna tofauti kubwa sana kati ya mjinga na mpumbavu.Mjinga ni mtu asiyefahamu jambo na anahitaji tu kuelimishwa.Kila mtu ana ujinga wake,hakuna mtu anayefahamu kila jambo.Mfano sio wote tunaoweza kuendesha meli,au kuongea kiyahudi n.k.Lakini Mpumbavu ni yule anayefahamu jambo lakini hafanyi.Mathayo 7:24-27 imethibitisha pia maana ya mpumbavu.

                                         


Mafanikio yako ya kimwili na kiroho yanategemea pia na watu unaojiwekea kwenye maisha yako.Zungushia maisha yako na watu chanya,wanaokuzungumzia vizuri kwa wengine,wenye upendo wa dhati sio kukupenda kwa sababu wanataka kitu fulani kutoka kwako,watu ambao wanaonekana na ni waelewa wakati wa uhitaji wako,mnamwomba Mungu pamoja katika roho na kweli, n.k.
Ondoa watu hasi katika maisha yako ambao hamnii mamoja,hamnyanyuani katika mambo mema, n.k Na hapa inabidi kuwa makini tena kama biblia inavyosema,wengine watakuja kwa gia hiyo hiyo kwamba ni wacha Mungu lakini matendo yao ndio yatakayokujulisha. (Mathayo 7:15-20 )

Kupata watu chanya katika maisha yako inahitaji uwe mtu chanya pia.Huwezi kuvutia watu chanya iwapo unakuwa hasi.Sio rahisi wema na ubaya kukaa pamoja au nuru na giza kukaa pamoja.Haiwezekani.Kuna ule msemo wa kiswahili unaosema 'Ndege wanaofanana rangi huruka pamoja'.Ni kweli.

1Corithians 15:33

33 Do not be deceived: “Bad company ruins good morals.”

Kwa lugha nyingine,makundi mabaya huharibu tabia njema.

Unapo-sense kwamba aliyekaribu na wewe sio yule uliyemdhania kuwa ndiye,Mtoe mkuku haraka kwenye maisha yako kabla hajaharibu tabia yako njema,kabla hajafuta ndoto zako njema.



2 Wakorintho 6:14-18
14 Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?

....kwa jinsi isivyo sawasawa ina maana gani?

Isivyo sawa sawa na Neno la Mungu au Maandiko na isivyo sawa sawa katika matendo.Ukiongozana na wavuta bangi,unaweza ukajizuia labda mwezi mmoja,lakini kadri siku zinavyosonga,utashagaa na wewe unaanza kuvuta bangi taratibu.Matendo ya mtu ndio kitu kitakachokujulisha uhalisia wake.

Ni watu wa aina gani umejizungushia katika maisha yako?

Kumbuka ukitaka urafiki na watu wema,mafanikio mazuri,kuwa na nguvu kiroho na kimwili,n.k ni lazima nawe uwe na tabia njema za namna hiyo  ili kuwavuta kwako maana matendo ya mtu ndiyo yanayomtambulisha na hapana urafiki kati ya haki na uasi,au nuru na giza.

Mpaka wakati ujao...

TANZANIA KWA YESU!

Friday, May 16, 2014

Adui Zangu Na Zako Ni Adui Za Bwana

 




Nini Maana Ya Adui?
Kamusi inaeleza ni mtu yoyote au kundi lolote lililo kinyume nawe.Chochote chema unachofanya hawataki,hawapendi,hawakifurahii,hawatoi ushirikiano,wanapinga mambo yako mema unayofanya. Kwa lugha nyepesi,Hakutakii Mema.

Lakini nyuma ya pazia,adui halisi ni shetani,siyo yule mtu/kundi linalotumika kinyume nawe.Ni muhimu sana kufahamu hili ili uweze kushinda.





Biblia pia ilitoa onyo kwetu sote,maana kuna wengine wanajificha katikati ya kundi la watu wa Mungu ukidhani ni wacha Mungu.Matunda au Matendo yao ndiyo yatakayokujulisha.
Mathayo 7:15-20
15  Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.

16  Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?
17  Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
18  Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
19  Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.
20  Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.
Biblia imezungumza wazi kuhusu adui.Hata shetani ambaye alikuwa kiongozi wa sifa Mbinguni amekuwa adui mkubwa wa Mungu.Kuliendeleza hilo shetani amekuwa akitumia watu wanaokuzunguka karibu karibu na kuwafanya wawe pingamizi la yale mema unayoyafanya.Kama yeye alivyokuwa karibu na Mungu kabla hajaharibu,ndivyo anavyotumia watu wa karibu yako,ili aharibu.Does that sound familiar?


Nini Cha Kufanya Unapogundua Adui Anakuzungukia?
Usipigane nae/nao katika ulimwengu wa kimwili,wala usilipe kisasi.Usipofanya hivyo,
 wewe utakuwa dhaifu,utashindwa.Hivi ni vita vya kiroho.Ingia kwenye maombi,mdunde shetani kisawasawa.Ukiweza unganisha maombi yako na mfungo,utaona shughuli ambayo Mungu ataifanya.Vita si vyetu,vita ni vya Bwana.



Kumbuka  vita vyetu si juu ya damu na nyama;bali ni juu ya falme na mamlaka,juu ya wakuu wa giza hili,juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho(Waefeso 6:11)

Biblia inasema nini basi kuhusu adui ?
  Kumbukumbu La Torati 28:7
7 Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.

Ayubu 8:22
22 Hao wakuchukiao watavikwa aibu; Nayo hema yake mwovu haitakuwako tena.

Isaya 54:15,17
15 Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.
17 Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.

Kumbukumbu la Torati 20:4
4 kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi.


Ipo mistari mingi mno kwenye biblia inayotueleza nini msimamo wa Mungu juu ya adui zetu.Lakini pia Bwana Yesu alisema jambo hili katika Matayo 5:44
44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi

Yes,ni ngumu kumeza lakini inawezekana.Kumbuka Stephano wakati anapigwa mawe anakufa alifanyaje?Aliwaombea waliokuwa wakimuua kwa mawe Matendo 7:54-60

Ukishayafahamu haya ni vyema kabisa kuyazingatia na kamwe vita inapoinuka juu yako haitakusumbua,tena utashangilia maana kwanza fahamu umemtia wivu shetani mpaka kafikia kukuchukia.Ujue sasa muda umefika wa kutumia silaha ulizonazo.



Tukutane tena wakati ujao..

TANZANIA KWA YESU!

Thursday, May 15, 2014

Kumwamini Mungu Na Kumtumaini



Yeremia 17:5,7
5  Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.
7  Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake.'
Haya maneno yametoka kwenye kinywa cha Mungu Mwenyewe.
Kumtegemea Mungu ni baraka na Mungu hupendezwa sana na mtu anayemtegemea.Kinyume cha hapo ni laana.Ukitaka kujua baraka na laana soma Kumbukumbu la Torati 28
Kupata hizi baraka kunaambatana kwanza na kumsikiliza Mungu kwa Bidii na Kutii.Kumbukumbu la Torati 28:1-2
Mungu ni halisi kabisa.Japo haonekani kwa macho lakini matendo yake yanaonekana dhahiri.Kuanzia uumbaji hivi vyote tunavyoviona mimea,watu,wanyama,n.k vyote ni yeye ameviumba.Wanadamu wote tumeumbwa na Mungu tena kwa mfano wake.Mwanzo 1:26
Mungu ana ratiba nzima kwenye kiganja cha mikono yake, ya maisha ya kila mmoja wetu na mipaka yetu anaijua(Isaya 49:16)
Mithali 3:5-7 inasema
'5  Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6  Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.
7  Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.'


Tunapotaka kufanya kitu chochote,ambacho kiko katika mapenzi ya Mungu,ni vizuri kumshirikisha na kumtumaini yeye tu kwa moyo wote.Hii inahusu hata zile nyakati za majaribu.Ukiweka tumaini lako kwa Bwana unakuwa na amani,furaha na nguvu za ziada ambazo zinakusaidia kusonga mbele.Utakuja tu kushangaa jaribu lako halipo tena.Mungu ameshakutoa humo.
Mithali 18:20-21 inasema hivi,
20  Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake.
21  Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.


Ni maneno gani unayojitamkia kila siku au unayotamka ukiwa unapitia hali fulani?Inabidi tuwe waangalifu zaidi maana vinywa vyetu vimeumbwa kwa mfano wa MUNGU.Vina uwezo wa kiuungu wa kuumba kila neno tunalotamka.Hata tunapoamka asubuhi ni vizuri basi baada ya kumshukuru Mungu kuanza kukiri chanya na kumtanguliza Mungu kuhusu siku hiyo kabla hatujatoka.Utaona utofauti mkubwa sana hata mambo yatakayokuwa yakiendelea siku hiyo utayamudu kirahisi zaidi tofauti na usipofanya hivyo mambo hayohayo yanakuletea 'stress'.
Kwa wale tunaolifahamu jiji la Dar es Salaam yani ukitoka nyumbani kwako tu ukaingia kwenye lami tayari foleni hii hapa.Unajua foleni tu inaweza ikaku-stress?unaanza kusonya kwenye gari,kununa by the time unafika mahali husika,huna mudi.Kitu kidogo tu umeshakwazika haswa unakasirika au kufoka.Lakini haya yote yanadhibitika kama ukimtumaini Mungu.Ile kumtanguliza tu Mungu asubuhi kabla ya kutoka inatosha kukufunika na uwepo wake popote.Hata hiyo foleni ataishughulikia.

Chochote unachofanya na lolote unalopitia,kuwa jasiri.Be strong in The Lord.Mungu hapendi waoga.Mi mwenyewe sipendi mtu mwoga mwoga.Na nguvu unaitoa wapi?Mungu akikufurahia.'The Joy of The LORD is our Strength'.
Tukutane tena wakati ujao..
Nakuacha na wimbo huu...
     Breathe by Michael W Smith



TANZANIA KWA YESU!


Monday, May 12, 2014

Kuendelea Kusimama Baada Ya Ushindi



Praise The Lord!...HalelujaaaaH!

Umepigana vita vilivyo vyema.Umeshinda.Ili tubaki kuwa washindi na kuendelea kushinda vita vingine vijavyo ni vyema kudumu kufanya yafuatayo..

1.Kudumu katika uhusiano mzuri na Mungu
Bila kuwa na mahusiano mazuri na Muumba wetu hatuwezi kushinda majaribu yoyote huku duniani.Vita ni vya Bwana.Pasipo Yeye sisi hatuwezi neno lolote Yohana 15:5

2.Ichukie dhambi,ikatae
Kaa mbali na dhambi.Dhambi isitajwe kwetu.Kumcha Bwana ni kuchukia uovu.Mithali 8:13
Je,unafahamu kwamba dhambi inafungulia milango ya shetani kuingia kwenye maisha yako na kukutesa.Ni muhimu sana kujitakasa kila mara maana kuna dhambi nyingine tunatenda bila kujua.1Yohana 1:8




3.Kudumu katika Kusali na Kuomba
Mathayo 26:41 Bwana Yesu alikuwa anawaambia wanafunzi wake umuhimu wa kukesha na kuomba.Kumbe kukesha na kuomba kunatufanya tuwe 'alert' kuona majaribu na hivyo kuweza kuyakwepa kabla hayajatufikia.

4.Kusoma Neno La Mungu
Neno la Mungu lijae kwa wingi mioyoni mwetu.Bila Neno hutaweza kumpinga yule mwovu.Bwana Yesu alitumia sana maandiko kumpinga yule mwovu Mathayo 4:1-11

Tukutane tena wakati ujao...tutaendelea

Nakuacha na wimbo huu ..(Mimi ni rafiki wa Mungu)..
Nampendaje Mungu?!!.We are good friends!Indeed!..Enjoy

I am a Friend of God by Israel Houghton....



TANZANIA KWA YESU!

Monday, May 5, 2014

Milango Mingine Hufunguka Kwa Kumtukuza Mungu Tu


Wengi wetu tumeshasikia au kusoma katika maandika habari ya Paulo na Sila.Walipofungwa gerezani licha ya wenzao kuwaombea,lakini wao waliamua kumwimbia Bwana katikati ya majaribu mazito.

Sifa,kuabudu na kushukuru Mungu katikati ya mambo unayopitia mpendwa ni jambo ambalo linauwezo wa kubadili hali unayoipitia ghafla.Ni vigumu sana kufanya haya pale unapokuwa kwenye mazito lakini Roho wa Bwana ni mwaminifu,atakuwezesha.

Nyimbo kama hizi za kumsifu,kumtukuza Mungu,zinazomkuza Mungu na kuthibitisha kwamba yeye ni mkuu na muweza kuliko jaribu lako,zina nguvu sana katika ulimwengu wa roho.

Mungu atusaidie,kumwona kwamba yeye ni mkuu,pale tunapopitia changamoto....

                                                             Agnus Dei-Michael Smith




                                                             Be Magnified-Don Moen

Be blessed... TANZANIA KWA YESU!

Yatupasa Kuvaa Silaha Kama Askari Vitani-2


Waefeso 6:10-18
10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.
11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,
15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

Njia pekee ya kuweza kusimama siku ya maovu au siku za kujaribiwa mtu ni kuwa umevaa hizi silaha wakati wote maana huwezi kujua ni siku gani utahitaji kuzitumia.

1.Kuvaa Kweli Kiunoni au Kuvaa mshipi wa Kweli
Kazi ya mkanda kiunoni ni kushikilia nguo isiachie ikaanguka pamoja na kukuweka nadhifu.Hivyo Kweli inatakiwa ivaliwe kiunoni kama mshipi ili kuweka silaha nyingine pamoja na kukupa unadhifu.Mtu akivaa mkanda anakuwa huru kukimbia,kuinama,kunyanyuka,kutembea n.k.Ndiyo maana Neno la Mungu likasema ifahamu Kweli nayo Kweli itakuweka huru.(Yohana 8:32).Kweli itakuweka huru na mambo yote kama ambavyo ukivaa mkanda unakuwa huru.Daima inakupa unadhifu katika maisha na kukusaidia mambo mengi sana.




2.Kuvaa dirii ya Haki Kifuani.
Kazi ya dirii ni kulinda au kukinga kifua ambacho kuna moyo ndani yake,dhidi ya mashambulizi.Vivyo hivyo inatakiwa Haki ikae kifuani mwako ili kukulinda na mambo yanayoweza kuuharibu moyo wako.Linda sana moyo wako...(Mithali 10:11-12)



 3.Kuvaa viatu vya Injili Ya Amani
Miguu ndiyo inayokupeleka kila mahali unapotaka kwenda.Hivyo kuvaa viatu vya amani inakusaidia wewe kuwa na amani kila mahali unapokuwa.Amani ya ndani ndiyo itakayokusababisha upigane vita vyenye akili,vyenye ujasiri na ushindi.Maana akili yako inakuwa na utulivu.Ndiyo maana kuna mtu anaweza akawa anapita kwenye jaribu kubwa,halafu unakuta ana amani tele.Hana wasiwasi hata sisi tunaomwangalia tunamshangaa wakati mwingine.Ndivyo ilivyo.Bila amani ya kweli kutoka ndani,huwezi kushinda majaribu.



4.Kuvaa Ngao Ya Imani
Ngao wakati wa vita au kupigana inasaidia kukinga dhidi ya mishale,mashambulizi ya adui.Vivyo hivyo Imani inatakiwa uitumie kama ngao yako.Yule mwovu anaporusha mishale dhidi yako usitetereke.Mwamini Mungu maana pasipo Imani haiwezekani kumpendeza Mungu.(Waebrania 11:6)



5.Kuvaa Chapeo ya Wokovu
Kitu cha thamani sana kwa mkristo ni wokovu wake.Askari vitani huwa anavaa chapeo au kwa lugha ya kawaida 'Helmet' kichwani ili kulinda kichwa chake dhidi ya mashambulizi.Ubongo,ufahamu wote upo kichwani.Wokovu wa mkristo ni jambo la thamani ambalo halipatikani mahali popote ila kwa Yesu Mwenyewe.Humo ndipo tunapopata kulinda mawazo,fikra,ufahamu na pia tumaini la kusonga mbele tukijua kuwa baada ya haya yote,tutaurithi uzima wa milele.



 6.Kushika Upanga wa Roho ambao ni Neno La Mungu
Upanga kazi yake ni kugawanya kitu.(Waebrania 4:12)
 '12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.'
Hii ni zaidi ya silaha!Yani bila Neno La Mungu HUWEZI kumshinda yule mwovu.Tunaona hata Bwana Yesu alipojaribiwa nyikani alitumia sana sana Neno la Mungu kumshinda Ibilisi.(Luka 4:1-13)Ndiyo maana tumeambiwa katika kitabu cha Waefeso 3:16 kwamba Neno La Mungu na likae kwa wingi mioyoni mwetu...




7.Kusali kila wakati katika Roho
Tunatakiwa kudumu katika maombi,tena tukisali katika Roho. Unajua,maombi ni ya muhimu sana.Ni mambo unayotaka kuongea sirini na Baba yako wa Mbinguni.Ndiyo maana mtu unatafuta mahali pa faragha kuomba.Hapo unakuwa umefanikiwa kuwakwepa watu wasisikie mazungumzo yako na Baba lakini shetani na mawakala wake wananyata kukusikiliza ili wakapange mikakati ya kukwamisha majibu na baraka zako zisikufikie kwa muda muafaka ikiwezekana wazikwamishe.(Daniel 10:13) Hapo ndipo kunena kwa lugha na kuongea katika roho kunapotengeneza 'privacy' ya kutosha.Kama umejazwa na Roho Mtakatifu na unanena kwa lugha,tumia sana lugha ya hiyo kuomba.shetani hawezi kamwe kung'amua mazungumzo yenu na Baba.Hata wewe mwenyewe akili zako hazitambui ni nini unaongea ila roho yako inafahamu vizuri sana.(1Wakorintho 14:14)
 '14 Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.'



Natumaini tumeelewa vyema sasa silaha za Mungu na namna ya kuzivaa ili tuwe washindi siku zote.

Mpaka wakati ujao...

TANZANIA KWA YESU!



Friday, May 2, 2014

Yatupasa Kuvaa Silaha Kama Askari Vitani


Hivi ulishawahi kuona askari anaenda vitani hajajitayarisha,hana silaha,kavaa suti na tai na ana uso mlegevu halafu akatoka ameshinda.Sidhani.Askari yoyote ni lazima apitie mafunzo,awe na mbinu,awe mkakamavu,awe na silaha ndiyo aende vitani akitaraji kwamba atashinda.Haiwezekani uende vitani kinyume na taratibu za uaskari halafu ushinde.Utadundwa kisawasawa!..kama sio kuuawa.

Vivyo hivyo katika ulimwengu wa roho.Tupo vitani wapendwa.Ibilisi na jeshi lake kila siku wanapanga mikakati ya kuturudisha nyuma ikiwezekana kutuangamiza kabisa.Yatupasa nasi kujipanga kukabiliana na jeshi hilo.Tayari sisi ni washindi katika Bwana maana kitendo tu cha Bwana Yesu kutufia msalabani tayari,ushindi ni wetu.Lakini hiyo haimzuii yule mwovu kutufuatilia,kama hujui haki zako,silaha ulizonazo,hujui kujitetea utaonewa sana na shetani.

Waefeso 6:10-13
10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.
11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.


Tunaona nini hapo?
1.Kuvaa silaha kunakufanya unakuwa hodari katika Bwana.Hivi ndugu yangu wewe ungependa kumuajiri askari muoga?Wa nini sasa?Unapotaka mtu wa kukusimamia jambo fulani,utataka mtu aliye hodari.Ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu.Anataka tuwe hodari katika YeYe.Ndio maana waoga ni watu wa kwanza kutupwa kwenye ziwa la moto.(Ufunuo 21:8)

2.Huwezi kuzipinga hila za shetani kama hujavaa silaha ZOTE za Mungu.shetani anashambulia maeneo tofauti tofauti ya maisha yetu kwa hiyo yatupasa kuvaa silaha zote za Mungu ili tuweze kumshinda

3.Unafahamu kuwa mambo mabaya ambayo yanaendelea kutuzunguka kwenye maisha yetu ya kila siku,adui yetu mkubwa siyo hao wanaotenda mabaya bali ni ufalme wa giza unawatumia?Kwa hiyo ili uweze kupigana na majeshi yaliyo nyuma ya pazia ni lazima uwe umevaa silaha zote za Mungu.Adui si wanadamu wanaotenda ule uovu,wao wanatumiwa tu kama chombo na ulimwengu wa giza.Adui ni shetani na jeshi lake.

4.Kuvaa silaha kunasaidia mimi na wewe kuweza kushindana siku ya uovu na kuendelea kusimama kuwa askari hodari badala ya kushindwa na kutoka ukiwa choka bovu;unatoka ukiwa shujaa na ukiwa upo juu.


Tukutane tena wakati ujao nitaendelea.......

TANZANIA KWA YESU!