Monday, May 5, 2014

Yatupasa Kuvaa Silaha Kama Askari Vitani-2


Waefeso 6:10-18
10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.
11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,
15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

Njia pekee ya kuweza kusimama siku ya maovu au siku za kujaribiwa mtu ni kuwa umevaa hizi silaha wakati wote maana huwezi kujua ni siku gani utahitaji kuzitumia.

1.Kuvaa Kweli Kiunoni au Kuvaa mshipi wa Kweli
Kazi ya mkanda kiunoni ni kushikilia nguo isiachie ikaanguka pamoja na kukuweka nadhifu.Hivyo Kweli inatakiwa ivaliwe kiunoni kama mshipi ili kuweka silaha nyingine pamoja na kukupa unadhifu.Mtu akivaa mkanda anakuwa huru kukimbia,kuinama,kunyanyuka,kutembea n.k.Ndiyo maana Neno la Mungu likasema ifahamu Kweli nayo Kweli itakuweka huru.(Yohana 8:32).Kweli itakuweka huru na mambo yote kama ambavyo ukivaa mkanda unakuwa huru.Daima inakupa unadhifu katika maisha na kukusaidia mambo mengi sana.




2.Kuvaa dirii ya Haki Kifuani.
Kazi ya dirii ni kulinda au kukinga kifua ambacho kuna moyo ndani yake,dhidi ya mashambulizi.Vivyo hivyo inatakiwa Haki ikae kifuani mwako ili kukulinda na mambo yanayoweza kuuharibu moyo wako.Linda sana moyo wako...(Mithali 10:11-12)



 3.Kuvaa viatu vya Injili Ya Amani
Miguu ndiyo inayokupeleka kila mahali unapotaka kwenda.Hivyo kuvaa viatu vya amani inakusaidia wewe kuwa na amani kila mahali unapokuwa.Amani ya ndani ndiyo itakayokusababisha upigane vita vyenye akili,vyenye ujasiri na ushindi.Maana akili yako inakuwa na utulivu.Ndiyo maana kuna mtu anaweza akawa anapita kwenye jaribu kubwa,halafu unakuta ana amani tele.Hana wasiwasi hata sisi tunaomwangalia tunamshangaa wakati mwingine.Ndivyo ilivyo.Bila amani ya kweli kutoka ndani,huwezi kushinda majaribu.



4.Kuvaa Ngao Ya Imani
Ngao wakati wa vita au kupigana inasaidia kukinga dhidi ya mishale,mashambulizi ya adui.Vivyo hivyo Imani inatakiwa uitumie kama ngao yako.Yule mwovu anaporusha mishale dhidi yako usitetereke.Mwamini Mungu maana pasipo Imani haiwezekani kumpendeza Mungu.(Waebrania 11:6)



5.Kuvaa Chapeo ya Wokovu
Kitu cha thamani sana kwa mkristo ni wokovu wake.Askari vitani huwa anavaa chapeo au kwa lugha ya kawaida 'Helmet' kichwani ili kulinda kichwa chake dhidi ya mashambulizi.Ubongo,ufahamu wote upo kichwani.Wokovu wa mkristo ni jambo la thamani ambalo halipatikani mahali popote ila kwa Yesu Mwenyewe.Humo ndipo tunapopata kulinda mawazo,fikra,ufahamu na pia tumaini la kusonga mbele tukijua kuwa baada ya haya yote,tutaurithi uzima wa milele.



 6.Kushika Upanga wa Roho ambao ni Neno La Mungu
Upanga kazi yake ni kugawanya kitu.(Waebrania 4:12)
 '12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.'
Hii ni zaidi ya silaha!Yani bila Neno La Mungu HUWEZI kumshinda yule mwovu.Tunaona hata Bwana Yesu alipojaribiwa nyikani alitumia sana sana Neno la Mungu kumshinda Ibilisi.(Luka 4:1-13)Ndiyo maana tumeambiwa katika kitabu cha Waefeso 3:16 kwamba Neno La Mungu na likae kwa wingi mioyoni mwetu...




7.Kusali kila wakati katika Roho
Tunatakiwa kudumu katika maombi,tena tukisali katika Roho. Unajua,maombi ni ya muhimu sana.Ni mambo unayotaka kuongea sirini na Baba yako wa Mbinguni.Ndiyo maana mtu unatafuta mahali pa faragha kuomba.Hapo unakuwa umefanikiwa kuwakwepa watu wasisikie mazungumzo yako na Baba lakini shetani na mawakala wake wananyata kukusikiliza ili wakapange mikakati ya kukwamisha majibu na baraka zako zisikufikie kwa muda muafaka ikiwezekana wazikwamishe.(Daniel 10:13) Hapo ndipo kunena kwa lugha na kuongea katika roho kunapotengeneza 'privacy' ya kutosha.Kama umejazwa na Roho Mtakatifu na unanena kwa lugha,tumia sana lugha ya hiyo kuomba.shetani hawezi kamwe kung'amua mazungumzo yenu na Baba.Hata wewe mwenyewe akili zako hazitambui ni nini unaongea ila roho yako inafahamu vizuri sana.(1Wakorintho 14:14)
 '14 Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.'



Natumaini tumeelewa vyema sasa silaha za Mungu na namna ya kuzivaa ili tuwe washindi siku zote.

Mpaka wakati ujao...

TANZANIA KWA YESU!



No comments:

Post a Comment